UKO SAWA.


Kama wewe ni mwananume anayependa wanaume, uko sawa!
Kama wewe ni mwanamke anayependa wanawake, uko sawa!
Kama ulizaliwa mwanamke na unajihisi kama mwanaume, uko sawa!
Kama ulizaliwa mwanaume na unajihisi kama mwanamke, uko sawa!


Kote duniani na katika nchi nyingi Afrika, Kenya pia, kuna kutoelewana kwingi na chuki dhidi ya watu ambao ni wasagaji, mashoga, wapenzi wa jinsia mbili, na wabadili jinsia.

Kwa majumba yetu na mijini na sana sana mitandaoni, kuna uwongo mwingi kuhusu watu ambao ni wasagaji, mashoga, wapenzi wa jinsia mbili, na wabadili jinsia. Hali hii inadhuru na kuwapa kiwewe wengi wa wasagaji, mashoga, wapenzi wa jinsia mbili, na wabadili jinsia na inafanya watu wengi kutuchukia. Lakini hapa kwa tovuti hii, sisi (kikundi cha wasagaji, wapenzi wa jinsia mbili, na wabadili jinsia) tuko hapa kubadilisha jambo hili. Tuko sawa! Na pia wewe uko sawa!

Tumeweka habari pamoja kukuonesha kwamba wewe kuwa mtu ambaye ni msagaji, shoga, mpenzi wa jinsia mbili, na mbadili jinsi ni sawa na kujibu maswali ambayo wewe au marafiki na jamaa zako wanaeza kuwa nayo.


Wasagaji, mashoga, wapenzi wa jinsia mbili, wabadili jinsia na wengineo ni kina nani?

Neno linalo eleza wanaume wanaopenda wanaume linajulikana kama shoga na neno linanoeleza wanawake wanaopenda wanawake ni msagaji. Watu wenye mvutio kwa wanaume na wanawake wanajulikana kama wapenzi wa jinsia mbili na wale ambao hawajihisi kama jinsia waliyopewa walipozaliwa wanaitwa wabadili jinsia.

Pamoja, lote huandikwa kama Wasagaji, mashoga , wapenzi wa jinsia mbili, na wabadili jinsia. Mara nyengine, ishara ya msalaba ‘+’ huongezwa kuwakilisha wengine wanaojitambulisha tofauti.

Tiba ya kuponya ushoga”  inadhuru na haijaungwa mkono na madaktari wanaotambulika na pia wanasaikolojia.”

Unastahili kuheshimiwa na kupendwa vile ulivyo. Kumbuka ya kuwa kila mtu ana haki ya kuwa vile alivyo. Watu wengine wanaweza kujaribu kukushawishi ubadilike lakini unavyojitambulisha ni ya kipekee na yenye dhamana. Mtu yoyote asijaribu kukubadilisha ulivyo. Kuwa msagaji, shoga, mpenzi wa jinsia mbili na mbadili jinsia ni maumbile na sehemu ya ajabu kwako wewe kama mwanadamu. Ni muhimu kujipenda na kujikubali jinsi ulivyo. Kujaribu kubadilisha maumbile yako na umpendaye inaweza kukudhuru na ni jambo lisilo la lazima. Kumbatia maumbile yako na ujihusishe na watu wanaokupenda na kukuunga mkono vile ulivyo.

Mara nyingi watu wanaotuzingira hujaribu kutuombea kwa sababu wanafikiri kuwa msagaji, shoga, mpenzi wa jinsia mbili na mbadili jinsia ni vibaya. Wengine wetu hupelekwa hospitalini au kutengwa kwenye makambi ili wabadilishwe.

Vitendo hivi mara nyingi hujulikana kama ‘tiba ya kubadili’ au ‘tiba ya kuponya ushoga’ na ni mbaya sana! Kulazimishwa kujaribu kubadilika (huwa haina mafanikio) huenda ikawakosesha raha watu ambao ni wasagaji, mashoga , wapenzi wa jinsia mbili, na wabadili jinsia. Pia inatupatia taharuki na kutufanya tuskie vibaya kujihusu. ‘Tiba ya kuponya ushoga’ inadhuru na haijaungwa mkono na madaktari wanaotambulika na pia wanasaikolojia.

Je, ni njia gani zinazodhuru ambazo ‘tiba ya kubadili’ hufanyika?

‘Tiba ya kubadili’ inaweza fanyika kwa njia tofauti zinazohusisha vurugu kihisia na kimwili na huenda ikawa vigumu kujulikana wazi. Njia zinazojulikana ni:

Kupelekwa kwa mwanasaikolojia atakayesema ubadilishe umpendaye na jinsi ulivyo.

Kuombewa nyumbani au kwenye madhabahu au kambini ambapo umetengwa ili uwache kujitambulisha ulivyo.

Kupewa adhabu kwa sababu ya hisia zako kwa kupitishwa umeme mwilini, kupigwa, kunyimwa chakula na vitu vyengine vya msingi.

Kwa nini ‘tiba ya kubadili’ inadhuru?

Mashirika mengi ya afya na mashirika ya afya ya akili duniani yamekashifu ‘Tiba ya kubadili’. Tiba hizi zinadhuru kwa sababu:

Hazijaungwa mkono na sayansi. Sayansi imeonesha ya kuwa wasagaji, mashoga na wapenzi wa jinsia mbili na wabadili jinsia SI wagonjwa na hawawezi kubadilishwa.

Watu ambao wanapitia ‘tiba ya kubadili’ hupitia huzuni, taharuki, matumizi ya dawa za kulevya na fikra za kujiua.

Madhara ya kupitia ‘tiba ya kubadili’ yanaweza kudumu kwa mda mrefu na kufanya iwe vigumu kwa wale walioponea kujithamini, kuamini watu, au kujenga mahusiano.

Watoto na vijana ndio wako kwenye hatari ya juhudi za kuwabadilisha walivyo.

Unaweza kufanya nini kama unahitaji msaada?

Tafadhali kumbuka ya kuwa kuwa msagaji, shoga, mpenzi wa jinsia mbili au mbadili jinsia ni sawa. Ni muhimu kupenda na kujikubali ulivyo.

Wasiliana na mashirika yanaowaunga mkono wasagaji, mashoga, wapenzi wa jinsia mbili na wabadili jinsia bila kujaribu kuwabadilisha.

Endelea kujifunza na kuwafunza wenzako kama wewe. Tuko na habari zaidi hapa chini unayoweza anza kusoma.

Maswali unayoweza kuwa nayo

Kuwa msagaji, shoga, mpenzi wa jinsia mbili au mbadili jinsia ni dhambi?


La, unavyojitambulisha haikufanyi mtenda dhambi. Watu huwa wanahisi tofauti kulingana na imani yao ya dini. 

Kwa bahati mbaya, viongozi wengi wa dini wanapinga wasagaji, mashoga, wapenzi wa jinsia mbili na wengineo. Wanasema huenda tunatenda dhambi na kudai kuwa tunataka kuharibu familia na kutulaumu kwa maafa ya asili kama mafuriko na ukame. Madai haya yote si kweli. Wasagaji, mashoga, wapenzi wa jinsia mbili na wengineo wanastahili kuthaminiwa, kupendwa na kupewa heshima kama mtu yoyote yule. Sisi ni watu halali kwenye familia zetu, makanisani na kwenye jamii.

Na makundi mengi ya dini na viongozi wanaunga mkono wasagaji, mashoga, wapenzi wa jinsia mbili na wengineo. Makundi mengi ya dini yanaamini kuwa mapenzi, wema na heshima ni muhimu kwenye mafunzo yao na wanatukaribisha kama watu muhimu katika mikusanyiko yao.

Hayati Desmond Tutu wa Cape Town alitangaza baada ya kukamilika kwa ubaguzi wa rangi mwaka wa 1994, vita dhidi ya chuki inayoelekezwa kwa wasagaji, mashoga, wapenzi wa jinsia mbili na wengineo ndio itakayopewa kipao mbele katika jitihada za kupigania haki nchini Africa Kusini. Alibishana ya kuwa chuki dhidi ya wasagaji, mashoga, wapenzi wa jinsia mbili na wengineo ni “uhalifu dhidi ya ubinadamu”

Nchini Uganda, askofu wa kiAnglikani Christopher Senyonjo alipigania haki za wasagaji, mashoga, wapenzi wa jinsia mbili na wengineo kwa kusema “Hufai kuumiza watu wala kuwapa adhabu kwa sababu ya jinsi walivyo.”

Kuwa msagaji, shoga au mpenzi wa jinsia mbili aliyeshikilia dini inaweza kuambatana, na watu wengi wamefanikiwa kusawazisha imani yao na utambulisho wao.

Nifanyeje kama mtu ninayemjali ni msagaji, shoga, mpenzi wa jinsia mbili au wengineo?


Jambo la maana mno unaloweza kufanya ni kumuunga mkono na kumkubali mtoto wako, ndugu, jamaa au rafiki. Haya ni mambo unayoweza kufanya kuhakikisha kuwa unayemjali anahisi amependwa, yuko salama na anaheshimiwa;

Unaweza kumwonesha mapenzi yasiyo na kifani na kumuunga mkono

Mweleze ya kuwa unampenda liwe liwalo na kuwa penzi lako kwake halitahathirika kwa sababu ya vile alivyo. Mwoneshe kwa maneno na vitendo ya kuwa umemkubali kabisa na kuwa vile alivyo haitabadilisha uhusiano wako kwake.

Unaweza kuskiza aliyoyapitia

Tengeneza nafasi ambayo atajihisi huru kueleza mawazo na hisia zake. Mskilize bila kumkatiza au kufika kwa hitimisho. Hii inaonesha ya kuwa unaheshimu maoni yake na uko tayari kumuunga mkono.

Unaweza kjifunza kuhusu masawala yanaowakumba wasagaji, mashoga, wapenzi wa jinsia mbili na wengineo na utambulisho wao.

Chukua nafasi kujua mengi kuhusu wasagaji, mashoga, wapenzi wa jinsia mbili na wengineo, utambulisho wao na maswala yao. Kuelewa wanayoyapitia yanaweza kukusaidia kuwaunga mkono vyema.

Unaweza kuunga mkono afya yake ya kiakili na pia anavyohisi

Muhimize kuongea kuhusu anavyohisi na anayoyapitia. Kama anahitaji, msaidie kupata wanasaikolojia wanaoweza kumuunga mkono na kuelewa maswala ya wasagaji, mashoga, wapenzi wa jinsia mbili na wengineo. Ushauri unaofaa unaweza kumsaidia kutatua changamoto zozote zinazomkumba.

Unaweza kusimama dhidi ya ubaguzi

Kama anabaguliwa au kuchokozwa, simama naye. Hii ni pamoja na kumtetea na kuhimiza shule yake, jamii na jamaa yake kuweka mikakati ya kumfanya ahisi amekaribishwa.

Unaweza kumsheherekea

Msheherekee alivyo na mambo muhimu maishani mwake. Kumwonesha kuwa unamuunga mkono kwa njia zenye maana zinaweza kuwaleta pamoja.

Heshimu safari yake

Katika harakati ya kumsheherekea mtu aliyejikubali, inaweza kuwa na majaribio kueneza habari kwa watu wengine wengi. Unaweza kuwa na nia nzuri ya kueneza habari hii lakini hiyo ni hadithi yake yeye mwenyewe kuisema. Kueneza hadithi yake inaweza kumhatarisha au kumfanya aishi na wasiwasi.

Sambaza